Jifunze Kutokana na Maombi ya Yesu

Yesu akasema, Baba, uwasamehe kwa kuwa hawajui watendalo (LUKA 23:34)

Ninaamini kwamba vile watu wanavyoomba na vitu wanavyoombea huonyesha mengi kuhusu tabia zao na ukomavu wa kiroho. Kuna wakati ambao maisha yangu ya maombi hayakuonyesha ukomavu mwingi wa kiroho. Hata ingawa nilikuwa nimezaliwa upya, nikawa nimejazwa Roho Mtakatifu na kufundisha Neno la Mungu, maombi yangu yalikuwa ya kimwili. Nilipoomba, nilikuwa na orodha ya matakwa ambayo nilifikiri lazima Mungu akubali ndiyo nifurahi- na vyote vilikuwa vya kawaida: “Bwana, fanya huduma yangu ikue. Tupatie gari jipya; fanya hiki; fanya kile. Fanya watoto wawe wenye tabia nzuri,” na kadhalika.

Kwa kujibu hilo, Mungu aliniambia tu, “Ninataka uchunguze maombi ya Yesu na maombi ya Paulo. Halafu tutazungumza kuhusu maisha yako ya maombi.” Bila shaka, kuna maombi mengi katika Biblia yote, haswa katika Zaburi, lakini Mungu aliniambia niombe maombi ya Yesu, ambayo hupatikana katika Injili, na maombi ya Paulo, ambayo yanapatikana katika Nyaraka.

Nilipoanza kuomba jinsi Yesu alivyoomba, niligundua kwamba hakuna njia nyingine yoyote yenye nguvu ya kuomba isipokuwa kuomba kwa kutumia Neno la Mungu kwa sababu linatuonyesha kilicho muhimu kwake. Aliomba maombi kama yale tulisoma katika andiko la leo na mengine mengi, pia ombi lake la “Wasafishe [chuja, takasa, watenge kwa ajili yako, wafanye wawe watakatifu] kwa ukweli; Neno lako ni kweli” (Yohana 17:17); ombi lake la umoja miongoni mwa watu wake (soma Yohana 17:23); na ombi lake kwa Petro: “Nimekuombea haswa wewe [Petro], kwamba imani yako [mwenyewe] isitindike” (Luka 22:32).

Ninakuhimiza kusoma Injili na kuona jinsi Yesu alivyoomba, halafu uombe vivyo hivyo unavyozungumza na Mungu na kumsikiliza.

NENO LA MUNGU KWAKO LEO:

Omba kwamba Mungu atafunua upendo wake kwako, na kwamba utautambua na kuujua.  

Facebook icon Twitter icon Instagram icon Pinterest icon Google+ icon YouTube icon LinkedIn icon Contact icon