Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake. —WARUMI 8:28
Kuna sababu nyingi sana za masikitiko, kuanzia kwa kusikitishwa kidogo hadi kurudishwa nyuma kabisa, na shetani anataka kutumia masikitiko katika maisha yetu ili kuiba furaha yetu. Anataka tuwe katika hali ya kutamauka ili tusipokee yote ambayo Yesu alikufa kutupatia.
Haijalishi sababu za masikitiko—za kimwili, kihisia, kiakili, au kiroho—mara tu tunapohisi masikitiko yakija, tunaweza kuchagua kuyapinga mara moja na kuchukua hatua yoyote ile ambayo Bwana anatuongoza kuchukua.
Mara tu tunapoanza kuhisi masikitiko (haswa likiwa suala linalotokea mara kwa mara), ni muhimu kwetu sisi kujiambia, Nitatazamia wema wa Mungu katika maisha yangu leo. Chochote kile ambacho huenda nimepoteza si kitu kikilinganishwa na kile nimepata ndani ya Yesu. Ukiwa na nia kama hii, itazuia hayo masikitiko kugeuka na kuwa utamaukaji na hata mfadhaiko.
Yesu alitupatia “vazi la sifa badala ya roho nzito” (Isaya 61:3). Hiki ni kitu tunachoweza kuchagua kuvaa badala ya kuzama katika kupoteza tumaini wakati ambao mambo hayafanyiki tunavyotaka. Kumpinga adui na kufanya uamuzi wa kudhamiria kumsifu Mungu kwa furaha tele hata katika nyakati ngumu itakuruhusu kushinda masikitiko na kuwa Mkristo mwenye nguvu kila siku.
Unapokosa hakika ya kile utakachofanya, simama kwenye neno la Mungu na ukiri ahadi zake juu ya maisha yako.