Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza… —ISAYA 43:2
Tunapojua kwamba Mungu yuko nasi, tunajua kwamba, tukiwa naye tunaweza kushinda matatizo yote. Hatuna lazima ya kuepuka matatizo. Tunaweza kukutana nayo ana kwa ana katika busara na nguvu za Mungu. Kitu chochote tunachotoroka au kujificha kutokana nacho bado kina nguvu juu yetu.
Wakati mwingine tunazunguka uo huo mlima, na kuishia kuwa kama Waisraeli jangwani ambao walizunguka kwa muda wa miaka arobaini (Kumbukumbu la Torati 2: 1-3). Lakini tunavyomkaribia Mungu, ndivyo tunavyozidi kufanya uamuzi wa kukabiliana na milima yetu na kwa ujasiri kuishinda pamoja na Mungu.
Hiyo tu njia ya ushindi. Daudi hakumtoroka Goliathi, alimkabili kwa jina la Bwana. Ninakuhimiza kukataa kuvunjika moyo hata kama hali zako zinaonekana ngumu kiasi gani. Amini kwamba Mungu ana mpango wa maisha yako, na uombe kwamba Mungu atakupa nguvu za kuzidi kupanda hata kama mlima wenyewe unaonekana kuwa mrefu kiasi gani.
La muhimu mno, ninakuhimiza kuamua kufurahia safari. Kufurahia maisha ni nia ya moyo, uamuzi wa kufurahia kila kitu kwa sababu Mungu anaweza kutumia vitu vyote—hata vitu vinavyoonekana kuwa vigumu—ili kuleta mpango wake mtimilifu.
Nguvu na uwepo wa Mungu katika maisha yako utakuinua juu ya hali ambazo wengine hawawezi kushinda.