Mungu Hutumia Aina Zote

Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na walimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe (WAEFESO 4:11-12).

Njia mojawapo ambayo Mungu huzungumza nasi ni kupitia kwa watu. Wakati mwingine watu hao ni marafiki au familia na wakati mwingine ni wachungaji, walimu, wainjilisti, mitume na manabii anaoweka katika maisha yetu. Mungu huwapa hawa watu karama ili kuwasaidia kujenga waaminiyo vile andiko la leo linavyosema, “kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu.”

Mojawapo ya karama ambazo Mungu amenipa ni karama ya kufundisha Neno lake. Ingawa karama yangu imekuwa baraka kuu katika maisha yangu, Mungu aliiweka ndani yangu kwa manufaa ya wengine.  Watu wengine huamua kwa sababu zozote ziwazo kwamba, hawanipendi, hawapendi namna ninavyofundisha, au hawaamini kwamba Mungu ameniita kutumika. Wanapofanya hivi, wanazima kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha yao, sio kupitia kwangu lakini kupitia kwa karama ambayo yeye mwenyewe amechagua kububujika kupitia kwangu.

Kilicho cha kweli kwangu ni cha kweli hata kwa watumishi wenzangu pia. Mungu ameweka karama za thamani ndani yao na kutakuwa tu na watu kila mara watakaofungua mioyo yao kwa karama hizi na wengine hawatafungua. Tunafaa kujifunza kupokea Neno la Mungu kutoka kwa watu tofauti. Tunakosea tunapotazama sana chombo ambacho Mungu amechagua kutumia kupitisha ujumbe kuliko ujumbe anaopitisha kwa kutumia chombo hicho.

Ninakuhimiza kumruhusu Mungu kukuzungumzia kupitia kwa yeyote anayechagua na kutopinga ujumbe kutoka kwake kwa kumpinga yeyote anayemtuma kukuzungumzia Neno lake.

NENO LA MUNGU KWAKO LEO:

Jifunze kufurahia watu tofauti na karama ambazo Mungu ameweka ndani yao kwa manufaa yako.   

Facebook icon Twitter icon Instagram icon Pinterest icon Google+ icon YouTube icon LinkedIn icon Contact icon