
Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Yoshua 1:6
Ujasiri ni sifa muhimu iwapo unakusudia kumfanyia Mungu mambo makubwa. Mara nyingi viongozi sio watu wanaokuwa na talanta sana, lakini ni watu walio na ujasiri. Huwa wanashukuru kwa kila nafasi mpya na kuchukua hatua wakati ambao wengine wanarudi nyuma kwa woga. Huchukua hatua za ujasiri kwa imani. Wakati mwingine wanaweza kukosea, lakini wakati mwingi huwa wako sawa kiasi kwamba huwa haijalishi.
Mungu hututarajia kuongezeka, kuzaa na kujaa (tazama Mwanzo 1:28). Hupendezwa na ujasiri; kwa kweli huidai kutoka kwa wale wanaofanya kazi naye. Bwana alimwambia Yoshua kwamba alikuwa achukue mahali pa Musa na kuwaongoza Waisraeli hadi kwenye Nchi ya Ahadi, lakini kulikuwa na sharti moja: Alitakikana kuwa na nguvu pamoja na ujasiri. Bwana alikuwa na Yoshua ili kumpa ujasiri aliouhitaji—na yuko nawe pia.
Sala ya Shukrani
Baba, nikiwa katika hali ambayo inaonekana kunishinda, ninakushukuru kwa kuwa tayari umenipa ujasiri ninaohitaji. Ninakushukuru kwa kuwa uko nami na sina cha kuogopa. Asante kwamba ninaweza kuwa na nguvu pamoja na ujasiri.