Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. —YOHANA 3:17
Mojawapo ya kifaa muhimu ambacho adui hutumia ili kujaribu kutufanya tuhisi vibaya ni hukumu, ambayo bila shaka inaweza kuwa sababu ya kukata tamaa. Kulingana na Neno la Mungu, sisi tulio ndani ya Yesu Kristo hatuhukumiwi tena, kushtumiwa wala kuhesabiwa makosa. Ilhali mara nyingi huwa tunajihukumu na kujishtumu.
Hadi nilipojifunza na kuelewa Neno la Mungu, niliishi sehemu kubwa ya maisha yangu nikihisi kuhukumika. Mtu aliponiuliza ni kitu gani kilinifanya nihisi kuhukumika, nilishindwa kujibu. Nilichojua ni kwamba nilikuwa na hisia isiyo dhahiri ya hukumu ambayo ilinifuata kila mahali kila wakati.
Kutokana na tajriba hiyo, Mungu alinipa ufunuo wa kweli kuhusu kutembea huru kutokana na hukumu na shutuma. Alinionyesha kwamba mimi na wewe kando na kupokea msamaha kutoka kwake, lazima pia tujisamehe. Lazima tuache kujichokesha akili kwa kitu ambacho amesamehe na kusahau (Yeremia 31:34, Matendo ya Mitume 10:15).
Ninaamini ni vigumu kukata tamaa ikiwa fikra zimewekwa chini ya udhibiti mkali. Ndiyo maana tunaambiwa katika Isaya 26:3 kwamba Mungu atatulinda na kutuweka katika amani kamilifu isiyokoma—iwapo mioyo yetu itamtegemea.
Mungu ana vitu vipya katika upeo wa maisha yako, lakini hutawahi kuviona iwapo utaishi na kurudia kuishi katika mambo yaliyopita.