. . . Mpende jirani yako kama nafsi yako. —MATHAYO 19:19
Ninaamini mojawapo ya shida kubwa ambazo watu wanazo leo ni vile wanavyohisi kujihusu. Watu wengi hupitia maishani wakiwa wamejidunisha na kujidharau. Mara nyingi, watu wamekuwa na haya mawazo mabaya kwa muda mrefu bila kutambua kwamba wanayo.
Unajifikiria vipi? Una aina gani ya uhusiano na wewe binafsi? Ninauliza kwa sababu kokote unakoenda, au unachofanya katika maisha haya, utakabiliana na wewe wakati wote. Hakuna kujihepa.
Bwana alituamrisha kupenda majirani zetu vile tunavyojipenda, lakini ni kitu gani kitakachofanyika iwapo hatujipendi? Hatuwezi kutoa tusichokuwa nacho. Mungu anatupenda na hilo linatupatia ruhusa ya kupokea upendo wake na kujipenda kwa njia ya kiasi. Wengi wetu hufikiri tumemchosha Mungu kwa makosa na dhambi zetu, lakini hilo haliwezi kufanyika.
Mungu huwa hakati tamaa juu yetu! Kadri tunavyomkaribia Mungu katika maisha yetu ya kila siku, ndivyo tunavyogundua vile tunavyopendwa kwa dhati, na ndivyo pia inakuwa rahisi kwetu sisi kuanza kujipenda.
Pokea upendo wa Mungu kwa ajili yako. Utafakari. Acha ukubadilishe na kukutia nguvu. Halafu uupeane.