Ee Mungu moyo wangu u thabiti. Nitaimba, nitaimba zaburi. —ZABURI 57:7
Ili kuona ushindi katika maisha yetu na kupata mafanikio makubwa kwa ajili ya Mungu, ni muhimu kwamba tuchague kuwa wakakamavu. Biblia inasema kwamba Yesu “aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu” (Luka 9:51), na tunaweza kufanya vivyo hivyo tunapomuishia Mungu. Iwapo tutatimiza kitu chochote cha maana, ni muhimu “kwa uthabiti na ukakamavu” tukazie uso wetu upande huo bila kukata tamaa.
Unapompokea Kristo kama Mwokozi na Bwana wako, Shetani atakupinga pande zote. Anataka ukate tamaa! Shetani hatatutandikia zulia jekundu tu kwa sababu tunaamua kumpokea Yesu. Lakini Yesu tayari amemshinda shetani. Shetani ni adui aliyeshindwa. Upinzani wake hauna nguvu ya kutosha iwapo uko karibu na Mungu, ukiwa unatembea katika nguvu zake na mapenzi yake juu ya maisha yako.
Usianguke katika mtego wa kufikiri kwamba lazima kila kitu maishani kinafaa kuwa rahisi kwetu. Omba usaidizi wa Mungu, pokea neema yake na udhamirie kutenda mapenzi ya Mungu, kuwa na mawazo mazuri na mwenye furaha, na kutembea katika amani ya Mungu hata mambo yawe vipi.
Chuchumilia mbele kwa ukakamavu mtakatifu, na mpango wa Mungu utatimizwa katika maisha yako.