Endelea kusonga Mbele

Endelea kusonga Mbele

Kwa sababu hiyo, nakukumbusha uichochee karama ya Mungu iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu. —2 TIMOTHEO 1:6

Katika maisha yetu ya kiroho, tunaweza kuwa tunapiga hatua kwa bidii au tunarudi nyuma. Hakuna kitu kama Ukristo uliotuama au uliokwama. Ni muhimu kuchuchumilia mbele. Ndiyo kwa sababu Timotheo aliagizwa kuchochea moto na kuamsha bidii ambayo wakati mmoja ilijaza moyo wake. Alikuwa amechoka, na moto ambao wakati mmoja uliwaka ndani yake ulikuwa umezima kidogo.

Ushahidi upo kwamba Timotheo alikuwa amepiga hatua moja nyuma, pengine kwa sababu ya woga. Bila shaka ni rahisi kuelewa kwa nini Timotheo alipoteza ujasiri na tumaini. Ulikuwa wakati wa mateso makuu, na Paulo, mlezi wake alikuwa jela. Ilhali Paulo alimhimiza Timotheo kwa nguvu kujichochea, kurudi njiani, kukumbuka mwito uliokuwa juu ya maisha yake, kupinga hofu, na kukumbuka kwamba Mungu alikuwa amempa roho wa uweza na upendo na akili timamu.

Wakati wowote tunaporuhusu hofu kututawala, tunaanza kurudi nyuma. Hofu hutuzuia kupiga hatua na kutufanya kutaka kugeuka na kukimbia badala ya kwenda mbele kwa bidii. Iwapo huna hakika, una shaka au hata una woga leo, pokea himizo la Paulo kwa Timotheo. Chochea imani yako, kuwa na moto kwa ajili ya Mungu, na usisahau kuwa yuko nawe. Ukiwa naye kando yako, hata vitu vionekane vigumu vipi, unaweza kufanya chochote unachohitaji kufanya kupitia kwake.


Usiwahi, Usiwahi, Usiwahi…Kukata Tamaa!

Facebook icon Twitter icon Instagram icon Pinterest icon Google+ icon YouTube icon LinkedIn icon Contact icon