Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu. —WARUMI 12:10
Kudhihirisha upendo wa Mungu ni zoezi la kila siku katika kuwatanguliza wengine. Tendo la kawaida la mwili wa binadamu ni kutomtanguliza mtu mwingine juu ya sisi wenyewe. Tunaelekea kushughulikia mahitaji yetu kwanza, lakini upendo hutuhitaji kubadilika na kuzoea kukutana na mahitaji ya wengine.
Kuruhusu mtu mwingine kuwa wa kwanza, au kusisitiza kwamba mtu mwingine achukue kitu kizuri sana kati ya vilivyopo, huhitaji mabadiliko ya kiakili kwa upande wetu. Huwa tunapanga kuwa wa kwanza, au kuwa na kizuri kushinda vyote, lakini upendo hubadilisha na kurekebisha—upendo huchagua kuwa wa pili badala yake. Tulikuwa katika haraka ya kufika tulikokuwa tukienda, lakini upendo huchagua kumtumikia mtu mwingine anayeonekana kuwa na hitaji kubwa zaidi.
Kadri tunavyomkaribia Mungu, ndivyo tunavyozidi kuwa na shina na msingi katika upendo (Waefeso 3:17). Kumtanguliza mtu mwingine kwanza ni zao la kuupokea upendo wa Mungu. Kadri tunavyopendwa zaidi ndivyo tunavyozidi kutaka kutoa upendo huo kwa wengine.
Tuna nafasi nyingi kila siku za kubadilika na kurekebika. Lakini tukifungika katika mipango yetu wenyewe, itakuwa vigumu kufanya hivyo. Ninakuhimiza kumwomba Mungu akusaidie kubadilika na kurekebika kwa moyo wenye furaha na nia nzuri. Muombe akusaidie kuwa na furaha na amani inayokuja kwa kuwapenda wengine.
Ni upendo wa Mungu tu unaoweza kutubadilisha kutokana na kuwa watu wabinafsi hadi kuwa watumishi wanyeyekevu wa Mungu na watu wengine.