Basi Mungu alimjalia Danieli kupata kibali na huruma… —DANIELI 1:9
Kisa cha Danieli na wana wa Kiyahudi kupata kibali mbele za mfalme wa Babiloni kinafahamika sana, lakini hatupaswi kukosa funzo la jinsi kibali cha kimiujiza cha Mungu kilivyokuwa nao baada ya kupelekwa mbali na manyumbani kwao na familia zao.
Kwa sababu ya dhambi zao dhidi ya Bwana, taifa la Yuda lilipelekwa utumwani Babiloni. Wakiwa huko, wale waliokuwa wakakamavu, akiwemo Danieli na marafiki zake watatu, walichaguliwa kuwa watumishi wa mfalme wa Babiloni. Kama sehemu ya miaka yao mitatu ya kipindi cha mafundisho, hawa barobaro walihitajiwa kula posho ya chakula cha mfalme na ya divai aliyokunywa. Hata hivyo, Danieli na rafiki zake waliazimu moyoni mwao kuwa hawatajitia unajisi kwa mlo huo na wakaomba kuruhusiwa kula mlo wao wa Kiebrania.
Walikataa kulegeza imani yao, na tunaambiwa ya kwamba Bwana alimpa Danieli “kibali, rehema, na huruma” mbele za matowashi. Wakapewa ruhusa ya kula mlo wao mradi tu haukuwadhuru. Bila shaka sio tu kwamba haukuwadhuru bali, uliwafanya kuwa wenye nguvu na afya zaidi na kuwafanya wateuliwe kama washauri walioaminiwa.
Simama imara katika imani yako na usiilegeze. Utatuzwa mwishoni!