. . . Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo… —KUTOKA 14:13
Yesu alisema kwamba, shetani ni mwongo na baba wa huo (Yohana 8:44). Ukweli haupo ndani yake. Hujaribu kutumia udanganyifu kudanganya watu wa Mungu ili waogope na kukosa ujasiri wa kuwa watiifu kwa Bwana na kuvuna baraka alizowawekea.
Mara nyingi hofu ya kitu ni mbaya sana kuliko kitu chenyewe. Iwapo tutakuwa wajasiri na tudhamirie kufanya chochote kile tunachokiogopa, tutagundua sio kibaya vile tulivyofikiria.
Kote katika Neno la Mungu, tunapata Bwana akiwaambia watu wake, “Msiogope.” Ninaamini sababu ya yeye kufanya hivyo ilikuwa kuwahimiza ili wasimruhusu shetani kuiba baraka yao.
Kwa njia hiyohiyo, kwa kuwa anajua tuna mwelekeo wa kujawa na woga, Bwana anaendelea kutuinua na kutuhimiza kuchuchumilia mbele tukishinda chochote kilicho mbele yetu ili tufanye mapenzi yake. Kwa nini? Kwa sababu anajua kuwa baraka kuu zinatungoja.
Adui anataka kukwambia kwamba hali yako ya sasa ni ithibati kwamba mustakabali wako hautakuwa na mafanikio, lakini Biblia inafundisha kwamba haijalishi hali yetu ya sasa ilivyo, hakuna lisilowezekana na Mungu (Marko 9:23).
Kuna ushindi kwa ajili yako iwapo utalifanyia hili neno moja mazoezi: Usiogope.