
Akaniambia, “Hilo ndilo Neno la Bwana kwa Zerubabeli, si kwa uwezo wala si kwa nguvu bali ni kwa roho yangu,” asema Bwana wa majeshi. ZEKARIA 4:6
Nilipigana na nafsi yangu kwa muda wa miaka mingi. Sikujipenda na nikajaribu kujibadilisha kila mara. Kadri nilivyong’ang’ana kubadilika, ndivyo nilivyofadhaika zaidi, hadi siku tukufu nilipotambua kwamba Yesu alinikubali tu vile nilivyokuwa. Yeye na Yeye peke yake tu ndiye angenifanya kile alichotaka niwe.
Usijidharau kwamba huwezi kutumika kwa sababu tu una baadhi ya udhaifu. Mungu humpa kila mmoja wetu nafasi ya kuwa mojawapo ya mafanikio yake. Udhaifu wetu humpa nafasi ya kudhihirisha uwezo na utukufu wake.
Badala ya kujichokesha ukijaribu kuondoa udhaifu wako, mpe Yesu na ushukuru kwamba anaenda kudhihirisha nguvu zake ndani yako. Ondoa macho yako kwa kile unachofikiri si sawa nawe na umtazame Yeye. Vuta nguvu zako kutoka kwa nguvu zake zisizoisha. Acha nguvu zake zijaze udhaifu wako. Huwezi kujibadilisha kwa mafanikio, lakini unaweza kumwamini Mungu kukufanyia.
Sala ya Shukrani
Ninakushukuru, Baba, kwamba sihitaji kufadhaika katika maisha yangu, nikijaribu kujibadilisha kwa nguvu zangu. Nisaidie kukupa udhaifu wangu leo, nikijua kwamba katika udhaifu wangu, unadhihirisha nguvu zako.