Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani kwenda. Na kulipokuwa jioni alikuwako huko peke yake (MATHAYO 14:23)
Kutumia muda wako peke yako na Mungu mahali patulivu ni muhimu kwangu na ninaamini pia ni muhimu kwako. Nina afisi nyumbani kwangu ninakoenda kila asubuhi kukutana na Mungu kabla ya kuanza siku. Isitoshe, karibu mara nne kwa mwaka ninapenda kwenda mahali kuwa peke yangu kwa muda wa siku chache. Ninafurahia na kuhitaji muda mtulivu wa kuwa na Mungu.
Watu wengi huchukua likizo kila mwaka na kupanga namna fulani ya burudani kila wiki. Tunataka burudani na utulivu, wala hakuna shida na hilo. Tunahitaji kufanya hivyo ili kudumisha maisha yenye afya na hisia zenye kiasi. Lakini kwa kweli tunahitaji zaidi likizo za kiroho na zinafaa kuwa kitu cha kwanza cha kuweka katika kalenda zetu za mwaka au taratibu zetu za wiki.
Hebu fikiria jinsi Mungu ataheshimiwa iwapo utaweka miadi naye kabla ya kuweka miadi ya kitu kingine chochote. Mimi huendesha makongamano Marekani na ng’ambo na kila mara huwa ninafurahishwa na idadi ya watu wanaosafiri na kuchukua likizo ili kuwa katika mojawapo ya makongamano haya. Huwa ninawasifu na ninajua kwamba Mungu anajivunia uteuzi wao. Watakua kiroho kwa sababu wanaacha shughuli zao nyingi ili kutumia wakati wao na Mungu.
Usingoje hadi matatizo au mkasa fulani ukudai kutumia muda wako na Mungu ili upate majibu kwa hali yako. Tafuta Mungu kwanza na kila mara, halafu utakuwa umeimarika tayari kiroho kuweza kukabiliana na chochote kijacho. Iwapo yesu alihitaji kuwa peke yake na Mungu Baba, bila shaka tunahitaji.
NENO LA MUNGU KWAKO LEO: Twaa kalenda yako sasa hivi na uratibu muda maalum wa kutumia na Mungu.