Basi Bwana ndiye Roho, walakini alipo Roho wa Bwana hapo ndipo penye uhuru (2 WAKORINTHO 3:17)
Ingawa tayari nimekwishataja katika kitabu hiki, jambo la ushikiliaji sheria kama kizuizi kwa maisha ya kuongozwa na Roho, ninataka nifafanue zaidi kuhusu jambo hili kwa sababu ninaamini ni kizuizi kikuu cha kusikia kutoka kwa Mungu.
Siamini kwamba tunaweza kuishi kwa furaha isipokuwa tuwe tunaongozwa na Roho wa Mungu, na hatuwezi kuongozwa na Roho na kuishi tukishikilia sheria wakati huohuo. Nia ya kushikilia sheria husema lazima kila mtu afanye kila kitu kwa njia ileile moja, kila wakati. Lakini Roho wa Mungu hutuongoza kila mmoja na mara nyingi kwa njia za pekee za kiubunifu.
Neno lililoandikwa la Mungu linasema kitu kimoja kwa kila mtu na halifasiriwi kama apendavyo mtu fulani tu (soma 2 Petro 1:20). Hili linamaanisha Neno la Mungu halisemi kitu kimoja kwa mtu mmoja na kingine kwa watu wengine. Hata hivyo, uongozi wa moja kwa moja wa Roho Mtakatifu ni jambo la kibinafsi.
Huenda Mungu akamwongoza mtu mmoja kutotumia sukari kwa sababu ya matatizo ya kiafya katika maisha ya mtu huyo. Hilo halimaanishi hakuna anayeweza kutumia sukari. Watu ambao ni washikiliaji sheria hujaribu kupelekea watu Neno la Mungu na kulifanya liwe sheria kwao.
Wakati mmoja nilisikia kwamba kufikia wakati wa kuzaliwa kwa Yesu, waandishi na mafarisayo walikuwa wamegeuza amri kumi katika kanuni elfu mbili za watu kufuata. Hebu fikiria kuishi chini ya sheria kama hizo. Huo ni utumwa!
Yesu alikuja kuwaweka wafungwa huru. Hatuko huru kufanya tunavyohisi kufanya, lakini tumewekwa huru kutokana na ushikiliaji wa sheria na sisi tuko huru kufuata Roho Mtakatifu katika njia zote bunifu za kibinafsi anazotuongoza kufuata.
NENO LA MUNGU KWETU LEO:
Mwamini Roho Mtakatifu kukuzungumzia na kukuongoza maishani.