Msamaha ni Muhimu

Nanyi kila msimamapo na kusali, sameheni, mkiwa na neno juu ya mtu; ili na Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu (MARKO 11:25)

Ikiwa tunataka kusikia kutoka kwa Mungu, lazima tu tuwe na mioyo safi tunapomkaribia- na njia moja ya hakika ya kuwa msafi mbele zake ni kuhakikisha ya kwamba tumemsamehe kila mtu alituumiza moyo au kutukosea. Msamaha si rahisi, lakini ni sharti la maombi yenye athari, vile tulivyosoma katika andiko la leo.

Hata ingawa wanafunzi wa Yesu walijua vizuri mafundisho yake kuhusu msamaha, bado waliupata ukiwa changamoto. Petro siku moja alimwuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara [mara nyingi hadi] saba? (Mathayo 18:21). Kimsingi Yesu alisema: “Hapana. Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.” Nambari saba huakilisha ukamilisho na utimilifu, kwa hivyo kile ambacho Yesu alikuwa anasema ni: usiweke mipaka yoyote kwenye msamaha; endelea tu kusamehe.”

Tunaposamehe, tunakuwa kama Yesu, tunatenda vile Mungu hutenda- kwa sababu ni Mungu anayesamehe. Msamaha hujidhihirisha kwa huruma; ni upendo katika matendo- sio upendo unaotegemea hisia, lakini upendo ulio na misingi yake katika uamuzi, uteuzi wa kimaksudi wa kumtii Mungu. Kwa kweli, ninaamini kwamba msamaha ndio sura kuu ya upendo. Msamaha na upendo ni chanda na pete na kuvidhihirisha hutoa heshima na utukufu kwa Mungu, hutuweka katika makubaliano naye, na kutufanya kutii Neno lake- ambalo hutusaidia kusikia sauti yake.

NENO LA MUNGU KWAKO LEO:

Kuwa na hakika ya kusamehe haraka, kila mara na kikamilifu.  

Facebook icon Twitter icon Instagram icon Pinterest icon Google+ icon YouTube icon LinkedIn icon Contact icon