Lakini kwa neema ya Mungu, nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake ilivyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi bali ni neema ya Mungu pamoja nami. —1 WAKORINTHO 15:10
Hakuna kitu kilicho na nguvu kuliko neema ya Mungu. Kila kitu katika Biblia—wokovu, ujazo wa Roho Mtakatifu, ukaribu na Mungu, na ushindi wote katika maisha yetu ya kila siku—unaitegemea. Bila neema, sisi si kitu, hatuna kitu, hatuwezi kufanya lolote.
Neema ya Mungu haitatizi wala haichanganyi. Kwa kweli ni rahisi sana kiasi kwamba wengi wetu hukosa kujua maana yake ya kweli na kuishia kufanya maisha yetu kuwa magumu. Ninajua nilifanya hivyo.
Kwa kusoma Neno la Mungu, nilianza kuona haja ya mabadiliko katika maisha yangu. Lakini sikujua kuwa neema ya Mungu ingeleta mabadiliko hayo. Sikujua jinsi ya kuruhusu Roho Mtakatifu kujaza maisha yangu na kusababisha vitu hivyo kufanyika. Kwa hivyo nikajaribu kujibadilisha na kubadilisha kila kitu katika maisha yangu kwa nguvu zangu. Matokeo yalivuka mipaka ya masikitiko na kuwa ya kuangamiza kihisia.
Nilipotambua neema ya Mungu niligundua kuwa nguvu zake zingeniwezesha kufanya kwa wepesi kile ambacho nisingefanya peke yangu. Ilibadilisha maisha yangu na inaweza kubadilisha yako pia.
Acha kila kitu unachofanya maishani kiwe “kwa neema kupitia kwa imani,” na utaishi kwa amani na furaha!