Yu Wapi Mungu?

Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, mwiteni, maadamu yu karibu (ISAYA 55:6)

Katika miaka yangu yote katika huduma, nimeulizwa kila mara, “Kwa nini siwezi kuhisi uwepo wa Mungu?” Wakati mwingine, huwa ninajiuliza swali hilo hilo.

Tunajua kutoka katika maandiko kwamba Roho Mtakatifu hatoroki na kutuacha tunapofanya kitu kisichompendeza (soma Waebrania 13:5). Kwa kweli amejitoa kukaa nasi na kutusaidia katika matatizo yetu, sio kutuacha katika matatizo hayo bila usaidizi.

La, Roho Mtakatifu huwa hatuachi, lakini huwa “anajificha” wakati mwingine. Ninapenda kusema kwamba wakati mwingine Mungu hucheza mchezo wa kujificha na kutafutana na watoto wake. Wakati mwingine hujificha kwetu hadi hatimaye, tunapomkosa ya kutosha, tunaanza kumtafuta. Na tunapomtafuta, anaahidi kwamba tutampata (soma 1Mambo ya Nyakati 28:9; Yeremia 29:13).

Katika Neno lake, Mungu hurudia kutuambia tumtafute- tutafute uso wake, mapenzi yake, na makusudio yake juu ya maisha yetu. Kutafuta kunamaanisha kuwa na hamu, kufuatilizia, na kufuata kwa nuvu zako zote. Tunashauriwa pia kumtafuta mapema, kwa bidii na jitihada bila kuchoka. Tusipomtafuta Mungu tutaishi maisha ya masikitiko. Kutafuta Mungu ni kitu anachotaka tufanye na kutuagiza tufanye; ni kitovu cha safari yetu naye na muhimu kwa maendeleo yetu ya kiroho. Mwambie Mungu jinsi alivyo muhimu kwako na kwamba huwezi kufanya lolote bila yeye.

NENO LA MUNGU KWAKO LEO:

Heshimu Mungu leo na kila siku kwa kumwambia ahusike katika kila kipengele na undani wa maisha yako.   

Facebook icon Twitter icon Instagram icon Pinterest icon Google+ icon YouTube icon LinkedIn icon Contact icon