Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu. —WAEFESO 3:20
Mungu anapenda kutumia watu wa kila siku wa kawaida ambao wana malengo na maono yasiyo ya kawaida.
Hivyo ndivyo nilivyo—mtu tu wa kawaida mwenye lengo na maono ambayo hutia moto bidii yangu. Lakini eti kwa sababu tu mimi ni mtu wa kawaida haimaanishi kwamba nimeridhika na wa kiasi tu. Sipendi hilo neno. Sitaki kuwa mtu wa kiasi. Sikusudii kuwa wa kiasi—na wala wewe usiwe.
Neno la Mungu linatuonyesha kwamba mtu yeyote anaweza kutumiwa na Mungu kwa nguvu kuu. Kadri tunavyomkaribia, ndivyo inavyowezekana kwetu kufanya mambo makubwa, mambo ambayo yanatushangaza hata sisi wenyewe. Tukiamini kwamba Mungu anaweza kututumia, na kama tutakuwa na ujasiri wa kutosha wa kuwa na malengo na maono yasiyo ya kawaida, Mungu atafanya mambo ya uweza mkuu ndani yetu na kupitia kwetu.
“Lengo lisilo la kawaida” ni kitu ambacho kinakaribia kutokuwezekana bila Mungu—ni zaidi ya yote ambayo tungetumainia, kuomba, au hata kufikiri kulingana na uweza wake mkuu unaofanya kazi ndani yetu. Hiki ndicho Mungu atakachofanya katika maisha yetu iwapo tutaamua kutokuridhika na kiasi.
Amua kupanua imani yako kwa kitu kikubwa. Tunaweza kuchagua kuwa watu wa kawaida walio na malengo yasiyo ya kawaida.